Ordo Virginum:mkutano wa kitaifa katika Jimbo Kuu la Torino,Agosit 25 hadi 28
Na Angella Rwezaula – Vatican.
“Waliowekwa wafu katika maelewano na Kanisa: utunzaji wa mahusiano,” ndiyo itakuwa mada itakayoongoza mkutano wa kitaifa wa Ordo Virginum,(watu waliokwa wakfu) ambao utafanyika Jimbo Kuu la Torino nchini Italia kuanzia tarehe 25 hadi 28 Agosti 2024 na kati ya washiki pia atakuwapo Kardinali Giorgio Marengo, Mwakilishi wa Kitume wa Ulaanbaatar nchini Mongolia na ambaye ni Mmisionari wa Consolata. Kwa mujibu wa waandalizi kwamba, wazungumza wawili watawaongoza wanawake hao, waliowekwa wakfu wa Italia katika siku nne za majadiliano na maombi katika nyumba ya Don Bosco, ya Valdocco huko Torino nchini Italia ambao ni Sr. Katia Roncalli, Mfransiskani na mhusika mkuu wa Udugu wa Evangelii Gaudium ambaye tarehe 26 Agosti 2024 atajikita na mada: “Kutoka katika mahusiano yanayotokana na Kristo hadi mahusiano yanayozalisha maisha na Askofu Mkuu Roberto Repole, wa Jimbo Kuu la Torino ambaye tarehe 27 Agosti 2024, atazungumza juu ya mada ya “Maisha ya kuwekwa wakfu na mahusiano katika Kanisa la jimbo.”
Utunzaji wa upendo
Tarehe 28 Agosti 2024 kutakuwa na meza ya mduara ambayo itaongozwa na mada: “Wanawake waliowekwa wakfu: utunzaji wa upendo wa udhaifu katika maisha ya kila siku,” ambapo Sr. Maria Silvia wa Shirika la Wadominikani wa Bethania(nyumba ya wafungwa ya Lorusso na Cutugno huko Torino-sehemu ya Wanawake), Sr. Elena Bernasconi (Wa shirika la watawa wa Mtakatifu Giuseppe Benedetto Cottolengo wa Torino) na Rosanna Tabasso wa (Fraternità della Speranza-Sermig-(Udugu wa Matumaini-Sermig). “Kwa kupatana na Njia ya Sinodi ya Kanisa la Italia inayojitayarisha kupata uzoefu wa awamu ya unabii, tumechagua kuimarisha mwelekeo wa ushirika katika Kanisa na umuhimu wa sisi pia kuwa, katika majimbo yetu, waendeshaji wa ushirika, kutunza mahusiano yote: na askofu wa Jimbo na masista wa (OV), na Jumuiya yetu tunayotoka, na wale wanaoshiriki nafasi zetu za kuishi na za kazi.” Hayo yalisisitizwa na wanawake wanne waliowekwa wakfu wa Kikundi cha Ushirikiano ambao, katika hafla ya mkutano wa kitaifa, wajipyaisha tena kwa miaka miwili ijayo. “Kujiweka wakfu kwetu kunatualika kuwa ishara ya furaha ya Injili katika ukawaida. Tunamshukuru Askofu Mkuu Repole na masisita wa Torino kwa ukarimu na msaada unaotolewa.”
Hija katika madhabahu ya Maria Consolata, Torino
Mpango wa mkutano huo pia unajumuisha hija ya ya Madhabahu ya Wakonsolata kwa ajili ya kumkabidhi Bikira Maria, na sala itakayoongozwa na Askofu wa Baraza lka Maaskofu Italia CEI kwa ajili ya sehemu hii ya Ordo virginum, Askofu Paolo Ricciardi, na ziara ya kutembelea Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane ambapo Bruno Barberis wa Chuo Kikuu cha Torino ataongoza mkutano kuhusu Sanda: kioo cha Injili na uchochezi kwa akili.” Ushiriki wa askofu wa Saluzzo, pia unatarajiwa. Cristiano Bodo, na Askofu msaidizi wa Tosrino, Mwashamu Alessandro Giraudo.
Nini maana ya Ordo Virginium?
Ndugu msomaji, nitumie nafasi hii kueleza kidogo kuhusu Ordo Virginium ni nini? Ordo virginum ina maana ya Shirika la mabikira au wanawake waliowekwa wakfu. Hawa ni Wakristo wanaojitoa kabisa, kwa sababu maisha yao yameelekezwa kabisa kwa Bwana, na wanapokea wakfu kutoka kwa Askofu, na wakiendelea kuwa katika maeneo yao wanayoishi. Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na Wakuu wa mashirika katika Mkutano Mkuu wa 82 wap USG uliofanyika Chuo Kikuu cha Wasalesinao kuanzia tarehe 27-29 Novemba 2013 aliwaeleza kuwa “Kazi ya pekee ya maisha ya kuwekwa wakfu ni kuweka hai ndani ya mbatizwa ufahamu wa tunu msingi za Injili, kushuhudia kwa namna ya ajabu na ya kipekee kwamba ulimwengu hauwezi kubadilishwa na kutolewa kwa Mungu bila roho ya Heri za mlimani.” Kwa njia hiyo, maisha ya kuwekwa wakfu daima huleta ndani ya dhamiri ya Watu wa Mungu hitaji la kuitikia kwa utakatifu wa maisha upendo wa Mungu unaomiminwa mioyoni na Roho Mtakatifu (rej. Rm 5:5), ukiakisi wakfu wa kisakramenti katika mwenendo, ilitokea kwa njia ya kazi ya Mungu katika Ubatizo, Kipaimara au Shirika. Kwa hakika, tunahitaji kuhama kutoka katika utakatifu unaowasilishwa katika sakramenti hadi utakatifu wa maisha ya kila siku. Maisha ya wakfu, pamoja na kuwepo kwake ndani ya Kanisa, yanajiweka yenyewe katika huduma ya kuweka wakfu maisha ya kila mwamini, mlei na mkleri. Kwa upande mwingine, isisahaulike kwamba watu waliowekwa wakfu pia wanapokea msaada kutoka katika ushuhuda wa miito mingine ili kuishi kikamilifu kushikamana na fumbo la Kristo na Kanisa katika nyanja zake nyingi. Kwa nguvu ya fadhila za utajiri huu wa pande zote, utume wa maisha ya kuwekwa wakfu unakuwa wa ufasaha zaidi na wenye ufanisi zaidi: kuonesha kama lengo kwa kaka na dada wengine, wakiweka mtazamo wao juu ya amani ya baadaye, furaha ya uhakika ambayo iko kwa Mungu.”
Waraka wa Kitume wa Papa Yohane Paulo II wa 25 Machi 1996 kuhusu Maisha ya Kitawa
Tutazame jambo jingine ambapo ilikuwa mnamo tarehe 25 Machi 1996, Papa Mtakatifu Yohane Paulo II, aliandika Waraka wa Kitume baada ya Sinodi, kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa, Maaskofu, vyama vya maisha ya Kitume, Taasisi za Kitume za kidunia na waamini wote kuhusu Maisha ya Wakfu na Utume wake kwa Kanisa na katika Ulimwengu. Katika moja ya vipengele, Papa aliandika kuwa: “Ni chemchemi ya furaha na matumaini kuona kwamba Shirika la kale la wanawali, lililoshuhudiwa katika jumuiya za Kikristo tangu nyakati za mitume, linashamiri tena leo hii. Wakiwekwa wakfu na Askofu wa jimbo, wanapata mafungamano ya kipekee na Kanisa, ambalo kwa huduma yao wanajitoa, huku wakibaki duniani. Hawa wanaunda sura maalum ya eskatolojia ya Bibi-arusi wa mbinguni na ya maisha ya baadaye, wakati hatimaye Kanisa litapata upendo kamili kwa Kristo Bwana-arusi" (rej.VC 7). Kwa njia hiyo Ordo virginum (Shirila la wanawali) ni aina shirika kongwe zaidi ya kuwekwa wakfu kwa wanawake katika Kanisa, iliyogunduliwa tena baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kutangazwa Ibada mpya, mnamo tarehe 31 Mei 1970, na kugunduliwa tena kwa uwezekano wa kuweka wakfu, ndani ya Kanisa mahalia kwa wanawake ambao wanabaki katika muktadha wao wa kawaida wa maisha ya kila siku.
Wawekwa wakfu mikoni mwa Askofu wa Jimbo
Hii ni aina ya maisha ya kuwekwa wakfu yenye sifa ya kuwekwa wakfu na Askofu mahalia kwa nia ya kubaki bikira na kujitolea kwa Kanisa mahalia. Uwekaji wakfu wa uhakika, makini na wa hadhara, unaopatikana katika muktadha wa hali ya kiroho ya Kanisa mahalia na hali ya kawaida ya maisha ya watu wa Mungu. Umaalum wa wanawali hao uliowekwa wakfu ni “ufadhili”, ambao “unapata thamani ya huduma katika huduma ya watu wa Mungu na kuingizwa watu waliowekwa wakfu katika moyo wa Kanisa na ulimwengu” (rej. Utangulizi wa Ibada ya Kuwekwa wakfu kwa Wanawali.) Chimbuko la kijimbo linamfanya aliyewekwa wakfu asikilize mahitaji mbalimbali ya Kanisa mahali ambalo, kuanzia Parokia yake, anajitoa kwa karama zake binafsi, hata bila kutekeleza utume maalum. Wanawake waliowekwa wakfu wanaishi 'mitindo' tofauti ya miito, lakini wanashiriki 'huduma' ile ile ya kuishi zawadi ya sadaka kamili kwa Bwana katika usafi wa moyo na kujitolea kwa ajili ya huduma ya Kanisa, kwa niaba na ndani ya watu wa Mungu, katika kawaida za hali ya maisha ya watu. Waliowekwa wakfu wana jambo la pamoja, la wakfu, na si kuwekwa wakfu kwa jumla, lakini ile maalum inayotazamiwa na kifungu na 604 cha Kanuni ya Sheria ya Kanoni; ukweli huu wa pamoja unamaanisha kwamba wanaunda Shirika, na kuwa ushirika wa madada (Ecclesiae Sponsae Imago, 110). Katika Taasisi za maisha ya wakfu kuna mambo mengine yanayofanana. Kwa mfano Taasisi ni kundi la waamini ambao wana mambo ya kiroho, makusudi na shughuli, utawala na maamuzi.
Namna ya kuishi maisha ya kiroho kwa njia ya mazungumzo na majadiliano na Askofu wa Jimbo
Mwanamke aliyewekwa wakfu, kwa upande mwingine, anachagua kwa hiari hali yake ya kiroho na kwa njia ya mazungumzo na majadiliano na Askofu wa jimbo, au mjumbe wake, anabainisha njia madhubuti za kutekeleza huduma yake kwa Kanisa, na pia kuandaa binafsi maisha kwa huduma ya kanisa. Kwa kawaida, wanawake waliowekwa wakfu wanaishi peke yao au pamoja na familia, na hawavai nguo au ishara tofauti. Wakati wa kuwekwa wakfu wanapokea pete na kitabu cha Liturujia ya Masifu, na wanaweza kupokea hat shela/au ishara nyingine kulingana na utamaduni na desturi Kila mtu aliyewekwa wakfu anaishi kujitolea kwake katika malezi ya kibinafsi kwa uwajibikaji. Askofu anaonesha umakini na wasiwasi wake kama mchungaji kwa ajili ya safari ya wanawake waliowekwa wakfu kwa kuhusika moja kwa moja na kupitia yale ya Msimamizi wa Ordo Virginamu, na kupitia wanawake waliowekwa wakfu ambao tayari wanasindikizwa na safari ya wanawake wengine, kwa mtindo wa kidugu na usawa. Huduma ya kichungaji ya Askofu inaelekea kuhakikisha kwamba kila mtu anaweza kupata msaada unaohitajika kwa ukuaji wa kweli wa kiroho na kibinadamu. Zana muhimu ni mikutano ya kila mwezi kwa watu wanaojiandaa kwa ajili ya Kuweka wakfu na kwa ajili ya malezi yanayoendelea. Kila mmoja amejitolea kuhakikisha kwamba Ordo virginamu inakuwa kwa kadiri iwezekanavyo mahali pa kukutana na majadiliano, ushuhuda na kujengana, kuthamini zawadi za kibinafsi na karama.
Mitindo ya kuwekwa wakfu(Kan 573 na Kan 576)
Kuna mitindo tofauti ya kujikita na maisha binafsi kwa Mungu. Ni wale walei waliowekwa kwafu au hata mabruda ambao wanapokea na kutelekeza ushauri kiinjili kwa njia ya kizingiti cha wakfu, kwa kuguka kuwa wajumbe wa Taasisi ya Maisha ya wakfu(Rej. Kan. 573 § 2). Aidha Taasisi za Maisha ya Wakfu ni vyama vya kikanisa vilivyochaguliwa, vimeridhiwa na kwa hekima vimeratibiwa na Kanisa kwa njia inayofaa ya sheria kuu na kwa namna ya pekee ( Kanuni, Katiba, (Regole, Costituzioni, Statuti) kwa sababu zinajitosheleza, na zinaweka nadhiri rasimu katika aina ya maisha ya kuwekwa wakfu (Kan.576). Ndugu msomaji kufikia hapo mmelewa nini maana ya Ordo virginium ambapo mara nyingi katika maeneo yetu ya kiafrika maisha haya hayajazoeleka, maana wengi wamezoa kuona watawa waliovaa shela tu, na kumbe kama tulivyona, bado kuna umati mkubwa wa wanawake wengi ambao wanavaa kama kawaida, bila hata ishara yoyote lakini wamewekwa wakfu chini ya Askofu na wanatoa huduma, ya kikanisa wakati wakikaa katika familia zao, au wengine wakichagua kukaa katika jumuiya wanayounda. Kwa upande wa Ulaya, Marekani, Amerika Kusini na kwingineko, aina hii ya maisha na mtindo wa Ordo Virginium umetanda zaidi kuliko nchi za bara la Afrika.