Tafuta

2024.02.07 Kambi ya Wakimbizi ya Wedweil Carine, Sudan. 2024.02.07 Kambi ya Wakimbizi ya Wedweil Carine, Sudan. 

Maaskofu Sudan/Sudan Kusini:Tunaamini viongozi wetu hawako tayari kwa amani

Maaskofu wanatoa wito kwa viongozi na watu wa Mungu nchini Sudan kusali na kusikiliza sauti ya Mungu na sauti ya watu.“Jukumu letu kuu kama Sudan Kusini,hatuwezi kujitenga na jirani yetu Sudan,tabia ya jamii ya Sudan imesambaratika,watu wametiwa kiwewe na kushtushwa na kiwango cha vurugu na chuki.”Maaskofu wanaomba mazungumzo kwa ajili ya amani na kulaani vitendo vibaya vya kihalifu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Maaskofu wa taifa  changa zaidi duniani walieleza kuhusiana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Sudan tangu mwaka 2023 kutokana na makabiliano kati ya viongozi wa Jeshi la Sudan (SAF) na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF) , na jinsi mzozo huo ulivyoharibu nchi kwa kiasi kikubwa hadi kufikia maangamizi karibu kabisa kwamba: “Jukumu letu kuu kama wa Sudan Kusini, hatuwezi kujitenga na jirani yetu Sudan, tabia ya jamii ya Sudan imesambaratika, watu wametiwa kiwewe na kushtushwa na kiwango cha vurugu na chuki.” Kwa njia hiyo Wajumbe wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki wa Sudan na Sudan Kusini(SSSCBC) walikusanyika hivi karibuni katika mkutano wa siku 3 mjini Juba.

MGOGORO WA SUDAN

Mgogoro huo, wa Sudan ambao kwa mujibu wa viongozi wa Kanisa “umesababisha uhalifu wa kutisha wa kivita na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na pande zote mbili, umesababisha watu wa Sudan kwenye janga la kweli la kibinadamu,” hivyo wito wa maaskofu kwa watu wa Mungu ni kutoa msaada kwa njia ya utoaji wa msaada wa kibinadamu, kazi ya utetezi kwa ajili ya amani, maandalizi ya baada ya vita katika suala la upatanisho, ukarabati, ujenzi na uponyaji kutokana na kiwewe na, zaidi ya yote, maombi.”

HAKUNA DALILI ZA MAZUNGUMZO YA AMANI

“Hadi sasa hakuna dalili hata kidogo ya mazungumzo ya amani ambayo yanaweza kuleta matumaini kwa Wasudan. Tunaamini viongozi wetu hawako tayari kwa amani. Mapambano na migogoro ndiyo yenye nguvu,” waliripoti maaskofu hao wakimnukuu Askofu Tombe Trille Kuku wa Jimbo la El Obeid ambaye katika ujumbe wake wa kichungaji alitoa taswira ya kutokuwa na hisia kwa pande zinazohusika katika kuruhusu amani kutawala Sudan, lakini badala yake wanachochea vita ambayo inasababisha mateso zaidi kwa idadi ya watu. “Wakati umefika kwao kufikiria juu ya watu na taifa. Kadiri mapigano yanavyoongezeka, ndivyo watu wanavyozidi kutawanyika na chuki kati ya makabila mbalimbali ya Sudan inaongezeka. Tupige  magoti ili tuombe na tusikilize sauti ya Mungu na sauti ya watu, ya watoto, ya wanawake wanaolilia amani, na pia damu inyomwagika juu ya ardhi ya watu wasio na hatia ambao walikufa katika moto . Mrudini kwenye mazungumzo kama watoto wa mama mmoja na baba mmoja.”

MAASKOFU WALAANI MAUAJI, UBAKAJI NA UPORAJI WA RAIA

Hatimaye, Maaskofu wa SSSCBC, wakichukua wito wa hivi karibuni ambao Baba Mtakatifu Francisko aliotoa baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Corpus Domini,(Mwili na Damu ya Yesu) kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro, walitoa mwaliko kwa pande zote kuweka  chini silaha na kuanza amani yenye maana,na mazungumzo huku wakilaani mauaji, ubakaji na uporaji wa raia na kudai uwajibikaji kwa uhalifu huo

25 July 2024, 16:10