Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa Marekani: Injili ya Uhai
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa ni kipindi cha katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayoadhimishwa na Jumuiya ya waamini wa Kanisa mahalia mintarafu Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kama njia ya kuendelea kuzungumza na Kristo Yesu katika safari ya maisha ya waamini. Ni muda wa kuimarisha katekesi kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Makongamano ya Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi angavu na endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo makini cha imani tendaji. Ni fumbo linalohitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kuzama na kugusa akili na nyoyo za watu. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 21 Julai 2024 limeadhimisha Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa lililofanyika kwenye Uwanja wa Lucas Oil. Huu umekuwa ni muda muafaka wa kuchochea moyo wa Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kuabudu Ekaristi Takatifu. Kimekuwa ni kipindi cha uponyaji wa ndani; toba na wongofu wa ndani. Katika maadhimisho haya Baba Mtakatifu Francisko aliwakilishwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Katika mahubiri yake ajilikita katika: Utume na zawadi; Uwepo hai wa Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai na mwisho ni Ekaristi na Umisionari. Baba Mtakatifu katika salam zake, amewataka watu wa Mungu nchini Marekani kujikita katika wongofu wa kiekaristi na wongofu wa kimisionari, kwa sababu wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kristo Yesu alitumwa na Baba wa milele kuyafanya mapenzi ya Baba yake wa mbinguni na kwamba Yeye ni Mkate ulioshuka kutoka mbinguni.
Ni katika muktadha huu, anasema Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle kwamba, umisionari ni zawadi na sadaka binafsi kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu: Kristo mwenyewe anasema, huu ni “Mwili wangu na hii ni Damu yangu” kwa ajili yenu. Kumbe, Ekaristi Takatifu ni mahali muafaka pa kuonja utume wa Kristo Yesu kama zawadi binafsi, mwaliko na changamoto kwa waamini kupata uzoefu na mang’amuzi haya ya kumwona Kristo Yesu kama kikolezo cha ujenzi wa umoja na mafungamano kati yao na hasa pale wanaposhiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya jirani zao! Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuishi mang’amuzi ya uwepo angavu wa Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai. Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Marekani anasema, Kardinali Christophe Louis Yves Georges Pierre, Balozi wa Vatican nchini Marekani katika mahubiri yake amegusia kuhusu Uamsho wa Ekaristi Takatifu unaohitaji kuambata na kukumbatia Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu inayopata chimbuko lake katika: Katekesi makini, Maandamano ya Ekaristi Takatifu pamoja na Ibada ya Misa Takatifu. Ni mwaliko wa kumwangalia na kumtambua Kristo Yesu katika maisha ya jirani zao. Huu ni ushuhuda kwamba, Kanisa la Kristo Yesu bado liko hai nchini Marekani.
Tafakari ya Kardinali Christophe Louis Yves Georges Pierre ilifanya rejea katika mahubiri ya Mtakatifu Yohane Krisostomo, kwa Kigiriki χρυσόστομος, Khrysóstomos, Mwalimu wa Kanisa anayewaalika waamini kumwabudu Kristo Yesu anayejionesha miongoni mwa maskini wanaoteseka kwa kukosa chakula, mavazi, makazi badala ya waamini kujikita katika mapambo ya nje; maskini ni Mahekalu hai ya Kristo Yesu. Askofu Tonino Bello anasema “kwa bahati mbaya, utajiri wa ajabu wa miji yetu hutufanya tuone kwa urahisi Mwili wa Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu katika madhabahu yetu. Lakini inatuzuia kuuona Mwili wa Kristo Yesu katika makazi ya maskini, wahitaji, wanaoteseka na wale wanaoelemewa na upweke hasi. Matokeo yake, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanakosa maana. Kumbe uamsho wa Ibada ya Ekaristi Takatifu nchini Marekani uende sanjari na utambuzi wa Kristo Yesu anayeteseka miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni wito na mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini; wakimbizi na wahamiaji pamoja na wale wote wasiokuwa na makazi ya kudumu! Ni mwaliko wa kuwalinda wote wanaoathirika kutokana na biashara haramu ya silaha na kujikuta wametumbukia katika vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Biashara haramu ya silaha duniani ni donda ndugu katika nchi nyingi duniani. Viongozi wa kidini wasimame imara katika kukuza na kudumisha: haki amani, ustawi na mandeleo ya wengi.