Caritas Italia:S.U.P.E.R,mpango wa kusaidia watu wa Ukraine
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mzozo nchini Ukraine unaendelea kuwa na athari mbaya kwa pande nyingi. Maeneo ya mashariki, ambayo yameathiriwa zaidi, bado yako katika hali mbaya ya kibinadamu. Kwa njia hiyo Mpango wa S.U.P.E.R - ‘Kusaidia Idadi ya Watu wa Kiukraine kwa Dharura na Urekebishaji’ unafadhiliwa na Wakala wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Italia (AICS) na kutekelezwa na Caritas Italia, Chama cha Kujitolea(VIS), Shirika la Wasalesian na vile vile pamoja na Caritas Spes, Caritas Ukraine, Caritas Poltava, Caritas Kamianske na Caritas Kharkiv. Maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao na uhaba wa chakula, maji, dawa na huduma za kimsingi bado ni mkubwa.
Jamii zinakabiliwa na changamoto
Jamii mahalia zinakabiliwa na changamoto kubwa za kijamii, ikiwa ni pamoja na kuenea kwa ukosefu wa ajira, kuongezeka kwa umaskini na kuenea kwa kiwewe cha kisaikolojia. Upatikanaji wa huduma za afya umekuwa mgumu zaidi kutokana na matokeo ya vita. Mgogoro wa wakimbizi umefikia kiwango kikubwa, na idadi inayoongezeka ya raia wa Ukraine wanaotafuta hifadhi katika mikoa mingine ya nchi.
Usaidizi wa dharura kwa watu wa Ukraine
S.U.P.E. R ya kusaidia Idadi ya Watu wa Kiukreni kwa Dharura na Urekebishaji – ni mpango wa euro milioni 1.9, unaofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Italia (AICS) kwa euro milioni 1.8 na Caritas ya Italia yenye euro 130,000. Mpango huu ni sehemu ya Mpango wa Dharura kwa wakazi walioathiriwa na mzozo wa Ukraine na nchi jirani (AID 012832) unaoongozwa na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Italia.
Kuokoa maisha katika maeneo yaliyoathiriwa
Kwa ufadhili wa Euro milioni 46.5, lengo ni kutoa msaada wa sekta mbalimbali wa kuokoa maisha katika maeneo yaliyoathiriwa moja kwa moja na migogoro na katika maeneo ya jirani yenye mkusanyiko mkubwa wa watu waliokimbia makazi yao. Kwa kushirikiana na asasi 27 za kiraia, mpango wa AICS unataka na kupanua mafanikio yaliyopatikana kwa Mpango wa Dharura wa Kwanza wa 2022-2023 (AID 012600), ambao ulitoa usaidizi kwa zaidi ya watu 20,000 kupitia miradi 14 kwa kuzingatia dharura, afya, elimu na ulinzi. Caritas Italiana, kupitia mpango wa SUPER, imejitolea kuboresha afya ya kimwili na kiakili ya jamii zilizoathiriwa na vita. Lengo kuu ni kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuhakikisha upatikanaji sawa wa huduma za msingi.
Watu wenye ulemavu na wanawake wanaoishi mazingira magumu
Mpango unahusisha mashirika kadhaa ya kiraia ya Italia na Ukraine, ikiwa ni pamoja na VIS (watu wa kujitoleoa, Shirika la Kimataifa la Maendeleo, Shirika la Wasalesian, Caritas mbili za kitaifa za Kiukraine, Caritas Spes, inayohusishwa na Kanisa la Kilatini, na Caritas Ukraine, inayoshirikiana na Kanisa Katoliki la Ugiriki, pamoja na Caritas tatu za jimbo la mtandao wa Caritas Ukraine: (Caritas Kharkiv, Caritas Poltava na Caritas Kamianske). Mpango huo unalenga watu walio katika mazingira magumu zaidi, ikiwa ni pamoja na watoto, wazee, watu wenye ulemavu na wanawake waliohamishwa, na kushughulikia changamoto za afya ya kimwili na kiakili zinazosababishwa na athari mbaya za migogoro.
Kukidhi mahitaji muhimu kufikia jamii zilizo hatarini
Usaidizi umebinafsishwa ili kukidhi mahitaji maalum ya kila kikundi, kwa kuzingatia hasa watoto wa umri wa shule na wazazi wao, kwa uangalifu maalum kwa wanawake, ambao mara nyingi hutengwa. Usaidizi unajumuisha utunzaji na usaidizi mahususi kwa watu wenye ulemavu wa rika zote, wakiwemo wakimbizi wa ndani kutoka maeneo yaliyoathiriwa na migogoro. Mapango huo unatekelezwa katika mikoa sita tofauti ya Ukraine: Dnipro, Poltava, Kharkiv, Zhytomyr, Lviv na Kiev, zikizingatia hasa maeneo ya vijijini na miji ya mikoa hii, ili kuweza kufikia jamii zilizo hatarini zaidi na zilizotengwa, ambapo hitaji la kusindikizwa ni kubwa zaidi.