Askofu Lazarus Msimbe SDS: Umuhimu wa Vyombo Vya Mawasiliano ya Jamii
Na Angela Andrew Kibwana, - Morogoro.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu ni chanzo na kilele cha mawasiliano, kwani anataka kuwasiliana na waja wake jinsi alivyo, kutoka katika undani wake. Kumbe, wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwasiliana kwa kutumia akili, moyo na mikono yao; kwa maneno mengine, haya ni mawasiliano yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha mawasiliano ni upendo wa Mungu ambao umemwilishwa kati ya waja wake. Mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa si matangazo ya biashara wala wongofu wa shuruti. Kanisa linakuwa na kupeta kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa yanafumbatwa katika ushuhuda; ukweli, uzuri na wema. Huu ndio ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; watu walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mawasiliano ndani ya Kanisa ni mchakato unaofumbatwa katika ujasiri pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa na hatimaye, kumezwa na malimwengu na hiki ni kishawishi cha Shetani, Ibilisi hata katika karne ya ishirini na moja. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu katika Sala yake ya Kikuhani, aliwaombea wafuasi wake, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwatakasa kwa ile kweli kwani Neno la Mungu ndiyo ile kweli. Wametumwa ulimwenguni lakini wao si wa ulimwengu huu. (Rej. Yoh. 17: 12-19).
Wadau wa tasnia ya mawasiliano wasishikwe na kishawishi cha kutaka kujifungia katika upweke wao, kwa kutaka kuendelea kubaki katika udogo wao. Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, wanahabari ni chumvi na chachu ya kuyatakatifuza malimwengu, kwa kuondokana na utamaduni wa watu kukata tamaa na kulalama kila wakati. Hata katika udogo na uchache wao, bado wanaweza kutenda makubwa kwa njia ya ushuhuda. Huu ni ushuhuda unaotangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya tunu msingi za maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu anasema, waandishi wa habari wanapaswa kutangaza ukweli wa Kikristo unaofumbatwa katika ukweli wa mambo, bila kuweka chumvi au kuwabeza wengine. Ndani ya Kanisa, watu wajisikie kuwa ndugu wamoja na watangaze uzuri. Hii ndiyo lugha ya mashuhuda wa imani na wafiadini, waliotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waandishi wa habari wawe mashuhuda wa Kristo kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, kama inavyoshuhudiwa katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Waandishi wa habari, wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili, changamoto changamani katika ulimwengu mamboleo.
Ni katika muktadha huu, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe SDS, wa Jimbo Katoliki Morogoro amepongeza uwepo wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania ambavyo vimeongeza chachu ya kuimarisha imani kwa waamini kupitia mchakato wa uinjilishaji unaofanywa na vyombo hivi. Uwepo wa vyombo vya habari vya Kanisa vinamsaidia kujiandaa vizuri katika mahubiri yake ili waamini waweze kulishwa Neno la Mungu kwa njia ya mahubiri na ushuhuda wa maisha. Kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii ujumbe wa Neno la Mungu unafika katika maeneo mengi ambapo viongozi wa dini si rahisi kufikia waamini wote kutokana na miundombinu ya kijiografia hivyo ameomba vyombo vya habari vya Kanisa kutafuta habari zinazogusa watu waishio pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Askofu Msimbe amesema kwamba vyombo vya habari vinapaswa kusimamiwa kwa uaminifu na uadilifu mkubwa; vinapaswa kuendelezwa na kutunzwa ili kuhakikisha vinasaidia kukuza mchakato wa uinjilishaji ili watu wengi zaidi waweze kufaidika na maisha na utume wa Kanisa katika medani mbalimbali za maisha. “Ninamshukuru Mungu kwa uwepo wa Vyombo vya Habari vya Kanisa kwa jimbo la Morogoro ninapata mrejesho mzuri kutoka kwa waamini ambao wanafuatilia vipindi na habari mbalimbali zinazolihusu Kanisa hivyo ni msaada mkubwa kwa imani za wakristo” amesema Askofu Msimbe. Amesema uwepo wa Radio Ukweli ya Jimbo Katoliki la Morogoro, Radio Maria Tanzania, Radio Tumaini, Gazeti Kiongozi, Jugo Media, na Radio Vatican: vyombo hivi vimesaidia waamini kupata habari za matukio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha ya Sala na Adili pamoja na mafundisho mbalimbali yanayowasaidia waamini kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Ameongeza kwamba kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari mara kwa mara katika ziara zake za kichungaji huambatana na vyombo vya habari vya Kanisa ili kuwezesha ujumbe wa Neno la Mungu kuwafikia waamini kwa haraka zaidi hasa waishio vijijini.
Ni fursa nzuri kupeleka ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii. Anasema awali alipata hofu kujua waandishi wa habari watapeleka ujumbe gani kwa watu endapo kama watarekodi kila kitu anachozungumza kwa njia ya mahubiri, hivyo ilimsaidia kujiandaa vizuri na kutetea chochote ambacho kitatangazwa na vyombo vya habari. “Kila ninapoongea najiandaa vizuri zaidi niweze kuongea ujumbe ambao utawafaa waamini na watu wote kwa ujumla, na kilichonipa nguvu ni kwamba Kristo Yesu mwenyewe alituambia tupeleke Habari Njema ulimwenguni kote, mimi kama mimi Askofu wa Jimbo siwezi kwenda ulimwenguni kote, ni vyombo vya habari ndivyo vinavyonisaidia kupeleka ujumbe wa Habari Njema ulimwenguni, ndio maana navutiwa na uwepo wa vyombo vya habari.” Ametumia fursa hiyo kuwahimiza waamini na watu wenye mapenzi mema kuchangia na kuviwezesha vyombo vya habari vya Kanisa ili viweze kujiendesha na kufanya utume wake kikamilifu. Idadi ya waamini wakatoliki kwa sasa Jimboni Morogoro ni 912,000 waamini hawa wengi wao wanakosa fursa ya kumwona Askofu mara kwa mara, ambapo kupitia vyombo vya habari vya Kanisa wanapata ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia ya Radio na magazeti ya Kanisa Katoliki. Sambamba na hayo askofu Msimbe amesema kuwa vyombo vya habari kwa ujumla vina mchango mkubwa katika kuhabarisha masuala mbalimbali ya kijamii, hususani kuibua matukio ya ukatili ikiwemo kupata ujumbe wa viongozi wanaokemea vitendo hivyo ili kudumisha maadili, amani na utu wema. Kufuatia vitendo vya matukio ya ukatili, serikali imekuwa ikihimiza viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kukemea vitendo hivyo, sambamba na kuwahimiza waamini kuishi maadili mema yatakayoliwezesha taifa kuwa na watu adili, wachamungu, wazalendo na hivyo kujenga na kudumisha: haki, amani, utulivu, maelewano; umoja na mshikamano wa Kitaifa.